Katika hatua ya kihistoria ya kuhakikisha usawa na ujumuishaji, mswada wa walemavu umeratibishwa rasmi leo na kufanywa kuwa sheria na hivyo kuondoa sheria ya mwaka 2003 iliyopitwa na wakati.
Sheria hii mpya inawakilisha hatua ya kipekee katika kuhakikishia walemavu haki zao pamoja na hadhi kote nchini Kenya.
Seneta Crystal Asige ambaye amekuwa akitetea haki za walemavu kwa muda mrefu alidhihirisha jinsi anajivunia kupitishwa kwa mswada huo kuwa sheria hatua anayotaja kuwa “Ushindi kwa ujumuishaji, usawa na haki.”
Akizungumza katika majengo ya bunge leo, Asige alisema, “Huu ni wakati wa kihistoria na wa mabadiliko kwa nchi yetu kwa walemavu. Pamoja tumeweka msingi wa mustakabali bora wa ujumuishaji.”
Sheria hii mpya inayowiana na katiba ya Kenya inaweka mfumo kamili unaolenga kulinda na kuwawezesha walemavu. Inatoa ulinzi faafu katika nyanja mbali mbali za maisha kama elimu, ajira, huduma za afya na uafikiaji ili kuhakikisha wakenya wote wanahusika kikamilifu katika jamii.
Seneta Asige,ambaye aliongoza juhudi za kupitishwa kwa mswada huo alishukuru wabunge wenza na watetezi wengine wengi waliounga mkono mchakato huo mzima.
“Bila sauti za kuunga mkono kutoka kwa wabunge wenzangu na watetezi wa haki za walemavu hatungeafikia ufanisi huu.” alisema Asige.