Rais William Ruto leo Jumatano amekuwa mwenyeji wa viongozi waliochaguliwa kutoka kaunti ya Homa Bay katika Ikulu ya Nairobi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Gavana Gladys Wanga, Waziri wa Fedha John Mbadi, Seneta Moses Kajwang, Mwakilishi wa Wanawake Joyce Atieno Bensuda, wabunge na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo.
Rais Ruto anasema wakati wa mkutano kati yao, walizungumzia miradi yenye kuleta mabadiliko inayotekelezwa na serikali kuu katika kaunti ya Homa Bay.
Suala lingine lililozungumziwa ni maandalizi ya sherehe za Sikukuu ya Madaraka itakayoandaliwa katika kaunti hiyo Juni 1, 2025.
Mkutano huo unakuja siku chache baada ya Rais Ruto kutia saini Mkataba wa Maelewano na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga.
Viongozi waliochaguliwa walioshiriki mkutano wa leo ni wanachama na wafuasi sugu wa ODM.
Tangu kutiwa saini kwa mkataba huo, viongozi hao wamekuwa mstari wa mbele kushabikia uongozi wa Rais Ruto na isitoshe wameahidi kumuunga mkono katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.