Rais William Ruto leo Jumamosi, amekamilisha ziara ya maendeleo ya siku tano katika eneo la Mlima Kenya, ambako alikagua miradi inayoendelea na kuzindua miradi mipya ambayo itachochea ukuaji wa kiuchumi wa eneo hilo.
Kiongozi wa taifa alikamilisha ziara yake ya Mlima Kenya, kwa kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa soko la kisasa la Githunguri, ambalo litawahudumia wafanyabiashara 1,200.
Rais alisema serikali yake imepiga hatua kubwa katika kuimarisha uchumi wa taifa hili, kwa lengo la kuinua maisha ya wakenya ambao kila uchao hujibidiisha kuboresha maisha yao.
Kuhusu ujenzi wa barabara ya Mau Mau, Rais alisema serikali imetenga shilingi bilioni 5, kufufua ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha kaunti za Kiambu, Murang’a, Nyandarua na Nyeri, huku kaunti ya Kiambu pekee ikitengewa shilingi bilioni 3.6 kwa mradi huo.
“Fedha zaidi zitatengwa kukamilisha ujenzi wa barabara zingine katika eneo hili,” alisema Rais Ruto.
Huku ziara hiyo ikiwa na ahadi kochokocho za miradi ya maendeleo, kiongozi wa taifa alidokeza kuwa serikali yake inatekeleza miradi 7 ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika kaunti ya Kiambu, kila mradi ukiwa na nyumba 16,000.

Na katika kutekeleza mpango wa kuimarisha uchumi kutoka chini almaarufu Bottom UP, Rais alisema masoko 25 ya kisasa yatajengwa katika kaunti ya Kiambu ili kuwapiga jeki wakulima na wafanyabiashara.
Akiwa katika kaunti ya Nyeri mapema leo Jumamosi, Rais alizuru ujenzi wa uwanja wa michezo wa Ruring’u, na kudokeza kuwa mzozo baina ya serikali na mwanakandarasi ulisababisha ujenzi wake kusimama, lakini sasa ujenzi huo utaendelea baada ya vikosi ya ulinzi nchini kuchukua usukani wa ujenzi.
“Mzozo wa kandarasi uliosimamisha ujenzi wa uwanja huu sasa umetatuliwa, na Vikosi Vya Ulinzi Nchini (KDF), vimechukua usukani wa ujenzi hadi ukamilike,’ alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa taifa aliwashukuru wakazi wa Mlima Kenya kwa kumkaribisha katika eneo hilo na kuweka kando siasa kandamizi ambazo alisema, zinahujumu ajenda ya maendeleo ya taifa hili.