Rais William Ruto amehimiza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA kutenga fedha katika hazina endelevu na ya kutegemewa kusaidia Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa, UNEP kutekeleza kazi zake ambazo ni muhimu.
Akihutubia mkutano wa 6 wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira, UNEA 6 huko Gigiri, Nairobi, Rais Ruto alihimiza wafadhili pia kuongeza michango wanayotoa kwa hiari, kwa kutambua ukubwa wa changamoto za sasa za kimazingira.
Alihimiza pia ushirikiano kati ya nchi zote ulimwenguni katika kutekeleza ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu kwani imesalia miaka sita tu kufanya hivyo.
Ana hofu kwamba ushirikiano huo usipokuwepo, basi ajenda hiyo haitatimia huku akisisitiza kwamba ni sharti la kila mmoja atambue jukumu lake katika ajenda hiyo ili kuweka bayana mchango wa kila mmoja katika kuafikia maono hayo ya pamoja.
“Ninasihi jumuiya ya kimataifa kuangazia uchumi usiodhuru tabianchi kwa vyovyote, unaofanikisha rasilimali na wa mzunguko,” alisema Rais Ruto huku akisifia UNEP kwa jukumu lake muhimu katika majadiliano kati ya serikali mbalimbali kuhusu mkataba wa plastiki wa ulimwengu mzima.
Rais Ruto alisema ulimwengu unastahili kukubaliana kwamba makao makuu ya mkataba huo yawe katika afisi za UNEP.
Alisisitiza kwamba ulimwengu unakumbwa na changamoto tatu kuu ambazo ni mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na viumbe hai na uchafuzi wa mazingira na taka za plastiki.
Kiongozi wa nchi alielezea imani kwamba mkutano wa UNEA 6 utakuwa hatua muhimu katika kuafikia jawabu la mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano wa 6 wa UN kuhusu mazingira almaarufu UNEA 6 ulianza Februari 26, 2024 na utafikia kikomo Machi mosi, 2024 katika makao makuu ya shirika la UNEP yaliyopo Gigiri, Nairobi.