Rais Museveni atangaza usaidizi kwa waliopoteza wapendwa kwenye mashambulizi ya waasi

Marion Bosire
2 Min Read
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ametangaza usaidizi wa kifedha kwa familia ambazo zilipoteza wapendwa wao kwenye shambulizi la waasi Jumatatu usiku katika eneo la Kamwenge.

Huku akitoa pole zake kwa familia hizo, Rais Museveni kupitia taarifa alisema ameelekeza mkuu wa matumizi ya fedha katika Ikulu kutoa msaada huo wa fedha kwa ushirikiano na mbunge wa kike wa eneo la Kamwenge.

Jumatatu usiku washambuliaji wanne ambao Rais Museveni sasa amewataja kuwa waasi kutoka Congo, walivamia eneo la msitu wa Kibaale na kuua watu 10 ambao wengi wao walikuwa walinzi wa mashamba.

Rais Museveni ameelezea kwamba washambuliaji hao wanne ni wanachama wa kundi la Njovu-Kamusu ambalo awali lilikuwa na wanachama 10 na wamekuwa wakitekeleza mauaji nchini Uganda.

Anasema kundi hilo ndilo lilivamia shule ya Nyabugaando ambapo waliua wanafunzi, wakaua watalii wawili na dereva wao na kuchoma lori lililokuwa limebeba vitunguu.

Kutokana na uchokozi wa kila mara wa waasi hao ambao wanalenga wananchi dhaifu wasio na hatia, Museveni ameelekeza wanajeshi watumwe katika maeneo ya mbuga za Queen Elizabeth, Semuliki na Bwindi na misitu ya Kibaale, Kyenjojo na Kagadi.

Wanahewa wa Uganda walivamia maeneo ya waasi hao kilomita 80 ndani ya mpaka wa Congo na Rais Museveni anasema majibu ya mashambulizi hayo yatafahamika baadaye.

Kiongozi wa Uganda ameahidi kuhakikisha waasi hao wanalipia maovu yao huku akitaka kukutanishwa na msichana aliyeepuka mashambulizi ya Jumatatu akimtaja kuwa jasiri.

Msichana huyo pia atapokea msaada ktoka kwa Rais Museveni.

Share This Article