Saa chache baada ya watalii wawili kuuawa na wanamgambo wa Allied Defence Forces ADF, Rais wa Uganda Yoweri Museveni amelaani mauaji ya wawili hao, aliosema walikuwa fungate.
Watalii hao wawili wa kigeni pamoja na dereva wao raia wa Uganda, waliuawa na gari lao kuchomwa moto katika Mbuga ya Kitaifa ya Malkia Elizabeth, inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Kitendo hicho cha magaidi hao kuwashambulia watu wasiokuwa na hatia, kilikuwa cha woga na cha kuhuzunisha kwa wapenzi hao ambao walikuwa wapya na kuzuru Uganda kwenye fungate yao,” alisema Museveni kwenye mtandao wa twitter.
Watalii hao walitoka Uingereza na Afrika Kusini, huku dereva wao akiwa ni raia wa Uganda.
“Ubalozi wa Uganda nchini Uingereza utawasiliana na familia ya watalii hao, na kutoa msaada wa aina yoyote utakaohitajika,” alisema Museveni.
Rais Museveni alilaumu mauaji hayo kwa wanachama wa Allied Democratic Forces (ADF), akiwataja “kundi dogo la magaidi wanaokimbia operesheni zetu nchini Kongo”.
Siku ya Jumapili, alisema vikosi vya Uganda vilifanya mashambulizi ya angani dhidi ya maeneo manne ya ADF nchini DR Congo, lakini akasema baadhi ya wanamgambo walikuwa wakijaribu kuingia tena Uganda.