Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, amepuuzilia mbali madai kwamba muungano huo unakumbwa na migawanyiko.
Kulingana na Odinga, habari hizo ni za kupotosha na zinakusudiwa kusambaratisha muungano huo.
Alisema viongozi wa Muungano huo wangali wana Umoja.
“Hakuna aliyeondoka katika muungano wa Azimio. Azimio ingali na Umoja isipokuwa wabunge kadhaa walioamua kuondoka chamani. Lakini uongozi wa Azimio uko pamoja,” alisema Raila
Raila aliyasema hayo akiwa katika kaunti ya Lamu kwa zoezi la kupigia debe chama cha Orange Democratic Movement (ODM).
Alidokeza kuwa muungano wa Azimio uko imara, huku akiwataka wafuasi wa chama hicho kupuuzilia habari hizo.
“Muungano wa Azimio hausambaratiki. Hatutaki vyombo vya habari kueneza propaganda,” alisema Waziri huyo mkuu wa zamani.