Kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga sasa anataka Mswada wa Fedha 2024 kuondolewa mara moja na badala yake majadiliano zaidi kufanywa kuhusiana na masuala tata.
Mswada huo umekuwa chanzo cha maandamano yenye vurugu ambayo yamesababisha vifo na kujeruhiwa kwa watu kadhaa. Kunao ambao wametekwa nyara katika njia ambayo imelaaniwa na taasisi kama vile chama cha wanasheria, LSK na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu, KNHCR.
“Mwanzo wa kusitisha mivutano hii na umwagikaji wa damu ni kwa serikali kuondoa mara moja na bila masharti Mswada wa Fedha na kutoa fursa ya mwanzo mpya na kufanyika kwa majadiliano,” alisema Raila aliyelalamikia kukandamizwa kwa vijana aliosema waliandamana kwa amani jana Jumanne.
“Wakenya watakumbuka kuwa tofauti zilipochipuka katika bunge lililopita kuhusiana na miito ya kupunguza kodi kwenye bidhaa za mafuta kutoka asilimia 16 hadi 8, serikali ya Jubilee wakati huo ilikubali kuondoa mswada huo na kutumia Sheria ya Fedha ya mwaka uliotangulia hadi makubaliano yalipofikiwa.”
Kwenye taarifa ya kurasa mbili, Raila pia ametoa wito kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, Umoja wa Afrika, AU na Umoja wa Mataifa, UN kuingilia kati hali nchini Kenya na kuokoa maisha na nchi hiyo.