Raila anawapotosha Wakenya kuhusu uchumi, asema Seneta Cherargei

Martin Mwanje
1 Min Read

Seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherargei amemshtumu kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga kwa kile alichokitaja kuwa kuwapotosha Wakenya kuhusiana na hali ya kiuchumi humu nchini. 

Raila amenukuliwa akisema anafikiria kuitisha tena maandamano mwaka 2024 kulalamikia gharama ya juu ya maisha.

Hata hivyo, Cherargei anamtaka kinara huyo wa Azimo kusema ukweli kwani uchumi wa nchi unaimarika taratibu na unatarajiwa kuwa thabiti mwakani. H

Akizungumza katika eneo la Kipchimchim, kaunti ya Kericho, Seneta Cherargei alisema hatakubali hatua zilizopigwa na serikali kufufua uchumi kuyumbishwa tena na maandamano.

Alisema ingawa nchi zingine zimeshindwa kulipa madeni, Kenya imechukua mwelekeo mzuri na imeweza kulipa madeni yake.

Alitoa mfano wa sekta ya kilimo aliyosema imeimarika na hivyo kuwafanya wakulima kupata mapato bora na kuchangia kuimarika kwa uchumi.

Awali, maandamano yaliyoitishwa na upinzani yalivuruga ukuaji uchumi huku baadhi ya Wakenya wakifariki na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia makabiliano kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama.

Kuna hofu kuwa hali sawia huenda ikashuhudiwa tena ikiwa upinzani utaitisha maandamano.

Share This Article