Kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga leo Jumanne amekutana na viongozi vijana kutoka Mlima Kenya katika hatua inayoonekana kulenga kuimarisha ushawishi wake katika eneo hilo.
Eneo la Mlima Kenya linajivunia mamilioni ya kura na linachukuliwa na wanasiasa wengi kuwa kiungo muhimu katika kuamua mshindi wa uchaguzi wa urais nchini.
Wakati wa mkutano wao, Raila anasema waliangazia suala la kupanda kwa gharama ya maisha nchini ambalo limekuwa mwiba kwa Wakenya walala hoi.
Masuala ya ufisadi na ugatuzi nayo pia hayakusazwa.
“Ufisadi, tuligundua unasalia kikwazo kwa maono yetu ya kiuchumi,” alisema Raila baada ya mkutano huo.
Mkutano huo ukija wakati Naibu Rais Rigathi Gachagua ameapa kufanya kila awezalo kuwaunganisha viongozi wote kutoka eneo la Mlima Kenya kwa lengo la kuwa na sauti moja kwa masuala ya kisiasa humu nchini.
Gachagua anachukuliwa kama kigogo wa siasa za Mlima Kenya hasa baada ya kuongoza kampeni zilizohakikisha muungano wa Kenya Kwanza unapata ushindi mkubwa katika eneo hilo wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.