Kesi dhidi ya kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu inatarajiwa kuendelea leo, baada ya kuahirishwa wiki iliyopita.
Kiongozi huyo wa chama cha CHADEMA anakabiliwa na mashtaka ya makosa ya uhaini na yale ya kusambaza habari zisizo za kweli.
Alhamisi Aprili 24, 2025, Lissu alikataa kuhusika katika kikao cha kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya mtandao katika mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Amezuiliwa katika gereza la Ukonga na kulingana na askari wa magereza aliyezungumza kutoka humo kwa njia ya video, Lissu alikataa kuingia kwenye chumba kilichotengewa uunganishaji wa kimtandao kwa sababu alitaka kufikishwa mahakamani Kisutu moja kwa moja.
Hakimu mkazi mwandamizi anayeshughulikia kesi hiyo Godfrey Mhini aliruhusu kesi hiyo ikaendelea bila uwepo wa Lissu lakini mawakili takribani 28 walikuwepo.
Kwa mara nyingine tena, makamu mwenyekiti wa CHADEMA bara John Heche amehimiza viongozi na wanachama wa CHADEMA wajitokeze mahakamani leo kufuatilia kesi ya mwenyekiti wa Chama hicho Tundu Lissu.
Ameitaka pia mahakama iendeshe kesi hiyo kwenye mahakama wazi na wala sio kwa njia ya mtandao kama wiki iliyopita, hatua ambayo inawanyima wengine fursa ya kuifuatila.
Akizungumza katika kongamano la waliokuwa wagombea wa chama hicho kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 huko Ukonga Jijini Dar es salaam jana, Heche alisema maeneo kama mahakama, hospitali na magereza yanafaa kutembelewa na umma.
Taarifa za awali ziliashiria kwamba kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 6, 2025, na hakimu Franko Kiswaga alielekeza kwamba itaandaliwa kwa njia ya mtandao.