Raia wa Uganda ahukumiwa kifungo cha miaka 5 jela kwa kutoa taarifa za uongo

Martin Mwanje
2 Min Read
Moses Kabali - Raia wa Uganda aliyehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela

Hakimu Mkuu wa mahakama ya Kahawa Gideon Kiage amemhukumu Moses Kabali kifungo cha miaka mitano jela nchini Kenya kwa kutoa taarifa za uongo. 

Ili kukwepa kifungo hicho, Kabali anaweza akalipa faini ya shilingi milioni tano.

Raia huyo wa Uganda alihukumiwa kifungo hicho baada ya kukabiliwa na mashtaka ya kutoa taarifa za uongo chini ya Sehemu ya 26 ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi Namba 30 ya mwaka 2012.

Kabla ya kufikishwa mahakamani, ilibainika kuwa Juni 30, 2024, Kabali alituma baruapepe kwa Sekretarieti Kuu ya Shirika la Polisi la Kimataifa la Interpol nchini Ufaransa akiitaka kuzitaarifu taasisi za usalama za Kenya juu ya shambulizi la kigaidi lililopangwa kutekelezwa humu nchini na kundi moja la kigaidi linalojulikana.

Kabali hasa alitaka Kitengo cha Polisi wa Kukabiliana na Ugaidi, ATPU kupashwa taarifa hizo.

Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI, raia huyo wa Uganda pia alidai kuwa watu wawili aliowafahamu, wakifanya kazi na makundi mengine yasiyofahamika ya kigaidi, walipanga kutekeleza shambulizi la kigaidi nchini Kenya kwa kutumia vilipuzi vya kujitengenezea, IED.

ATPU ilianzisha uchunguzi kuhusiana na suala hilo ambapo watu kadhaa walihojiwa na hatimaye Moses Kabali kukamatwa  Septemba 3, 2024 katika eneo la Eastleigh.

Baada ya upekuzi wa simu mbili za mkononi, tarakilishi mbili na nyaraka kadhaa, ilibainika kuwa ni Kabali aliyetuma baruapepe kwa Sekretarieti Kuu ya Shirika la Polisi la Kimataifa la Interpol nchini Ufaransa.

 

Share This Article