Maafisa wa polisi jijini Nairobi wamemkamata raia wa India anayehusishwa na ulaghai wa uwekezaji wa dhahabu wa takriban shilingi milioni 172.3.
Mshukiwa huyo ni Maheshbhai Rameshbhai Bhadra.
Alinaswa alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kutoka Dubai.
Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imesema mshukiwa huyo alikamatwa baada ya mwekezaji kulalamika kulaghaiwa fedha kupitia mfumo wa malipo wa Hawala, uliohusisha mawakala huko Dubai na Kenya.
“Uchunguzi umebainisha kuwa mlalamishi alihadaiwa kutuma pesa ili apate kilo 210 za dhahabu, lakini hilo halikutimizwa,” ilisema DCI kupitia ukurasa wa X.
Mshukiwa huyo anazuiliwa wakati akisubiri kufikishwa mahakamani.
DCI ilisema haitalegeza kamba katika kukabiliana na ulaghai wa fedha na kuwakamata wanaowapunja wawekezaji fedha zao.