Polisi wawakamata washukiwa watano wa wizi wa kimabavu

Tom Mathinji
2 Min Read

Maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa watano wanaoaminika kuhusika na visa vya wizi wa kimabavu kwenye barabara kuu ya Thika- Nyeri na Thika – Embu.

Washukiwa hao walikamatwa baada ya msako mkali kutekelezwa na maafisa wa asasi mbali mbali kwa usaidizi wa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kutoka Gatanga.

DCI kupitia ukurasa wa X, imesema washukiwa hao wamekuwa wakijisingizia  kuwa maafisa wa polisi wa trafiki  na maafisa wa Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA), nakusimamisha magari kabla ya kuwashambulia madereva, kuwaweka pingu na kisha kuwaibia bidhaa wanazosafirisha.

Kwenye tukio moja mifuko jumla ya unga wa mahindi 450 iliibiwa kutoka kwa lori moja lilikuwa likisafirisha bidhaa hiyo hadi Nairobi ilhali lori jingine lililokuwa likisafirisha bidhaa ya Colgate yenye thamani ya shilingi milioni 5.4 lilitekwa nyara nakisha kupatikana huko Embu.

Washukiwa wakuu walikuwa wamekamatwa awali huko Ruiru na mtaa wa South B, ambako makachero walipata sare za jeshi, bastola bandia, pingu na vifaa vingine vilivyoaminika kutumika kuwashurutisha waathiriwa.

Washukiwa wengine 3 Khalid Abdirahman Mohammed, Shueb Ahmed Hussein na Yusuf NurnAbdullahi, walikamatwa mtaani Eastleigh Jumanne walikopatikana na unga ulioibiwa.

Idara ya DCI imesema inawasaka washukiwa zaidi huku ikiwataka madereva kuwa macho na kuripoti watu wanaowashuku kuwa maofisa bandia wa serikali katika barabara kuu.

Kulingana na idara hiyo, wanawasaka wanachama wawili wa genge Hilo ambao wako mbioni.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article