Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, leo Alhamisi ameongoza shughuli ya kuteketeza mihadarati ya thamani ya shilingi bilioni 8.2, katika kiwanda cha simiti cha Bamburi, kaunti ya Mombasa.
Murkomen alisema zoezi hilo la kuharibu mihadarati hiyo ni hatua kubwa ambayo imechukuliwa na taifa hili katika vita dhidi ya utumizi na ulanguzi wa dawa za kulevya.
“Tunaimarisha ulinzi kwenye mipaka yetu, kusambaratisha mitandao ya ulanguzi, kuziba mianya ya kisheria na kufuata mali iliyopatikana na fedha za uhalifu,” alidokeza waziri Murkomen.
Mihadarati hiyo iliyoteketezwa aina ya methamphetamine yenye uzani wa kilo 1,000, ilinaswa mwezi Oktoba mwaka 2025 na maafisa kutoka asasi mbalimbali za usalama katika bahari hindi.
“Hatutalegeza kamba hadi tutakapokabiliana na zimwi hili ambalo linaharibu familia, vijana na kuchochea ongezeko la uhalifu wa kupangwa,” alisema Murkomen.
Zoezi hilo pia lilishuhudiwa na maafisa wa ngazi za juu wa usalama, akiwemo Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Manaibu wake Gilbert Masengeli na Eliud Lagat na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya jinai (DCI) Mohamed Amin, miongoni mwa wengine.