Polisi wasaka waliomuua mhudumu wa bodaboda na kunajisi mkewe Homa Bay

Marion Bosire
2 Min Read

Polisi katika kaunti ya Homabay, wanawasaka magaidi waliomuua mhudumu wa bodaboda na kunajisi mkewe. Tukio hili lilijiri katika tarafa ndogo ya Namaji mashariki, kijijini Rateng B saa 4 usubuhi ya jumanne ( 28/5/2024).

Kwa mujibu wa chifu wa tarafa ndogo ya Lambwe Mashariki Bernard Onditi, magaidi hao walilenga kumuibia mwendazake pesa za mchango alizopata kutoka Kwa wahisani kwa lengo la kununua pikipiki mpya ambayo hakuwa amenunua kwani aliamua kukarabati yake ya kawaida.

Katika uvamizi huo, marehemu alikatwa kwa shoka na kunajisi mkewe aliyejifungua hivi karibuni. Ni katika vurumai hiyo ambapo majirani walisikia na wakaja kumsadia hatua iliyofanya wezi hao kutoroka na pikipiki na simu kisha kuvitupa vichakani vilipogunduliwa na wanakijiji.

Wahasiriwa hao walipelekwa katika hospitali ya mafunzo na rufaa ya kaunti hiyo ambapo alifariki dunia wakati mkewe akipokea matibabu.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Mbita, Solomon Barng’etuny alihakiki kisa hicho na kusema kuwa polisi wameanzisha uchunguzi.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha maiti cha hospitali hiyo ukingoja upasuaji.

Hii ni mara ya pili marehemu kuvamiwa na kuibiwa pikipiki.

Juma lillilopita, wahudumu wa bodaboda walifanya maandamano mjini wakilalama kuhusu ongezeko la visa vya wengi wao kushambuliwa.

Mwenyekiti wao Richard Opiyo alisema kuwa wenzao watano wameuwa hivi karibuni.

Share This Article