Mahakama yatoa kibali cha kukamatwa kwa Seneta Mandago

Martin Mwanje
2 Min Read

Seneta wa kaunti ya Uasin Gishu Jackson Mandago ametakiwa kujisalimisha kwa polisi.

Hii ni baada ya mahakama ya Nakuru kutoa kibali cha kukamatwa kwake.

Mandago anatuhumiwa kwa kufuja mamilioni ya pesa ya wanafunzi waliotarajiwa kuenda kusomea katika nchi za Canada na Finland alipohudumu kama Gavana wa kaunti hiyo.

Wanafunzi hao pamoja na wazazi wao wamekuwa wakifanya maandamano mjini Eldoret na kwingineko kushinikiza kuwajibishwa kwa waliofuja pesa zao.

Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS inasema imekuwa ikimsaka Mandago tangu jana Jumanne lakini juhudi zao hazijaambulia chochote kwani Seneta huyo ameenda mafichoni.

“Huduma ya Kitaifa ya Polisi ipo katika mchakato wa kutekeleza kibali cha kumkamata Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago, ambaye ameenda mafichoni tangu jana, na inatoa wito kwa Seneta huyo kujisalimisha kwa kituo cha polisi kilichopo karibu,” ilisema NPS katika taarifa leo Jumatano.

“Aidha NPS inatoa wito kwa raia walio na ufahamu wa alipo Seneta Mandago kupiga ripoti kwa kituo cha polisi kilichopo karibu nao au kupiga ripoti kupitia nambari zisizotozwa ada ambazo ni 999, 112, 911 na nambari ya kufichua habari kwa idara ya ujasusi wa jinai ya DCI ambayo ni 0800722203.”

Huku maafisa wa usalama wakimsaka, Mandago amesema kwenye mtandao wa Twitter kwamba anafahamu maafisa wa DCI wanamtafuta akielezea kuwa yuko tayari kujisalimisha punde atakapotakiwa kufanya hivyo.

“Kuna uvumi kote mjini Eldoret kwamba maafisa wa DCI wamekuwa wakinitafuta usiku kucha. Kama raia anayetii sheria, nitajitokeza punde nitakapotakiwa kufanya hivyo. Nimekutana na uongozi wa wazazi na kukubaliana mwelekeo wa kuchukuliwa kama walivyoeleza katika taarifa yao kwa vyombo vya habari jana jioni,” alieleza Mandago.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *