Naibu Rais Rigathi Gachagua aliyetimuliwa madarakani na Bunge la Seneti kwa mara nyingine amepata pigo mahakamani.
Hii ni baada ya jopo la majaji watatu lililoteuliwa na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kukataa kujiondoa kwenye kesi ya Gachagua anayepinga kutimuliwa kwake.
Majaji hao ni Eric Ogola anayeliongoza jopo hilo, Anthony Mrima na Dkt. Freda Mugambi.
Gachagua, kupitia mawakili wake wakiongozwa na Paul Muite, jana Alhamisi aliwataka majaji hao kujiondoa kwa misingi kuwa wana uhusiano na upande wa washtakiwa kwenye kesi hiyo.
Alitoa mfano wa jinsi majaji hao walivyoonyesha wazi kuwa na upendeleo katika uamuzi wao juu ya iwapo Naibu Jaji Mkuu alikuwa na mamlaka ya kuteua jopo hilo kusikiliza kesi hiyo.
Katika kutaka majaji hao wajiondoe, Gachagua alidai kuwa mkewe Jaji Ogola aliteuliwa na Rais William Ruto kwenye taasisi moja ya serikali na kwa misingi hiyo Jaji Ogola ataupendelea upande wa washtakiwa.
Ruto ni mhusika kwenye kesi hiyo.
Jaji Mrima alidaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na Spika wa Bunge la Seneti Jeffah Amason Kingi.
Ingawa Gachagua alitaka majaji hao wote wajiondoe, hakumnyoshea kidole cha lawama Jaji Mugambi.
Upande wa washtakiwa ukiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa zamani Prof. Githu Muigai ulipuuzilia mbali madai hayo ukiyataja kuwa yasiyokuwa na msingi.
Gachagua amekuwa akikumbwa na pigo moja baada ya jingine tangu aanze kupinga kubanduliwa kwake madarakani, mapigo yaliyoanzia kwenye Bunge la Taifa na lile la Seneti.
Mabunge yote mawili yaliidhinisha kutimuliwa kwake madarakani.
Ombi lake la kupinga Naibu Jaji Mkuu kuteua jopo hilo la majaji watatu pia lilipingwa na mahakama.