Tumieni msimu wa mvua kupanda miti, Mama Taifa Rachel Ruto awarai wanafunzi

Martin Mwanje
2 Min Read
Mama Rachel Ruto akiwa a viongozi wengine katika Ikulu ya Nakuru, wakati wa Tuzo za Mazingira (FLAMA) 2025.
Mama Taifa Rachel Ruto ametoa wito kwa wanafunzi kutumia msimu wa mvua unaoendelea kupanda miti na kurejesha mfumo ikolojia kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha, ametoa wito kwa wanafunzi kupanda miti na mimea ya matunda nyumbani kwao, shuleni na katika taasisi kwa lengo la kukabiliana na athari kubwa za uharibifu wa mazingira.
Rachel aliyazungumza hayo katika Ikulu ya Nakuru, wakati wa Tuzo za Mazingira (FLAMA) 2025.
“Leo, tunaposherehekea washindi wa Tuzo za Mazingira 2025 Mazingira, hatukabidhi tu vikombe, tunakabidhi tochi  —  tochi ya uwajibikaji, ubunifu, na uongozi wa mashujaa vijana wa taifa hili,” alisema Mama Taifa.
Aliongeza kuwa FLAMA ilizinduliwa mnamo mwaka 2023 kwa maono rahisi — kuwasaidia wanafunzi vijana kuwa na maono ya kiubunifu na kuelezea mazingira kupitia macho na mawazo yao.
“Lengo lilikuwa kuwapa watoto jukwaa la kujifunza, kupenda na kuongoza katika masuala ya utunzaji mazingira. Maono hayo yamekua tangu wakati huo na kuwa vuguvugu linaloleta pamoja zaidi ya shule 2,000 na kufikia takriban wanafunzi milioni moja katika kaunti zote 47.”
Alisema Kenya inakuza kizazi kipya cha mashujaa vijana wa mazingira.
“Tunapowakabidhi waototo wetu jukumu, wanatimiza jukumu hilo. Watoto wetu siyo tu viongozi wa kesho — wao ni wanamageuzi wa leo,” aliongeza Mama Taifa.
Alisema upanzi wa miti unapiga jeki mpango wa “Jaza Miti” wa Rais William Ruto unaolenga kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032 ili kupunguza gesi chafuzi kwa mazingira.
Website |  + posts
Share This Article