Kiongozi wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis amemfuta kazi mkosoaji wake mkuu ambaye amekuwa akihudumu kama askofu wa kanisa hilo nchini Marekani kwa jina Joseph Strickland.
Strickland ambaye anafahamika sana kuegemea upande wa kihafidhina yaani conservative amekuwa akikashifu uongozi wa Papa Francis katika kanisa hilo.
Afisi ya Papa haikuelezea zaidi kuhusu hatua hiyo ya kufuta askofu kazi ikitizamiwa kwamba viongozi wa kanisa Katoliki wasumbufu huelekezwa au kushauriwa kujiuzulu.
Hata hivyo mwakilishi mmoja wa Papa nchini Marekani ameelezea kwamba hatua hiyo inahusiana na uchunguzi ulioamuriwa na Papa Francis kuhusu uongozi wa Dayosisi ya Tyler aliyokuwa akisimamia Strickland jimboni Texas.
Askofu Strickland anaongoza kundi fulani la waumini wa kanisa katoliki nchini Marekani ambao wanapinga mabadiliko anayotekeleza Papa Francis.
Amekuwa akiingilia mipango ya Papa Francis ya kubadili msimamo wa kanisa Katoliki kuhusu masuala yanayoathiri jamii kama uavyiaji mimba, haki za watu waliobadili jinsia na ndoa za watu wa jinsia moja.
Mwezi Julai alionya kwamba ukweli fulani wa kimsingi wa kanisa Katoliki ulikuwa unapingwa kama kile alichokitaja kuwa kudunishwa kwa familia kama ilivyokusudiwa na Mungu kuwa kati ya mwanaume na mwanamke pekee.