P Diddy arejesha ufunguo wa jiji la New York

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki na mfanyibiashara Sean Combs maarufu kama P Diddy amerejesha ufunguo wa jiji la New York kulingana na ombi la Meya wa jiji hilo Eric Adams.

Ombi hilo lilitolewa kufuatia kuvuja kwa video ya kamera za CCTV iliyomwonyesha Diddy akimpiga mpenzi wake Cassie Ventura mwaka 2016 katika hoteli moja.

Meya Adams alimtumia Diddy barua ya kuomba arejeshe ufunguo huo aliozawadiwa Septemba mwaka jana baada ya kukwazwa na video hiyo ya Diddy na Cassie.

Katika barua hiyo, Adams alisema kwamba anasimama na wahanga wote wa dhuluma za kijinsia na kifamilia akiongeza kusema kwamba kamati inayohusika na utoaji wa funguo hizo iliamua kumpokonya Diddy ufunguo wake.

Funguo hizo za mwigo hutolewa kwa wakazi wa New York ambao mchango wao katika jamii ni mkubwa. Diddy alirejesha ufunguo huo Juni 10, 2024 kulingana na taarifa kutoka kwa afisi ya Meya wa jiji la New York.

Mwanamuziki huyo ametajwa kwenye kesi zipatazo 8 za aina mbali mbali za dhuluma ambapo anadaiwa kudhulumu watu kingono na hata kupiga wengine.

Wakati shirika la CNN lilitoa video inayomwonyesha akimpiga Cassie, Diddy alichapisha video kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii akiomba msamaha.

Website |  + posts
Share This Article