Mwanamuziki na mtayarishaji wa muziki Sean Combs maarufu kama P Diddy ameomba msamaha kwa kumshambulia aliyekuwa mpenzi wake Cassie Ventura mwaka 2016.
Hii ni baada ya shirika la utangazaji la CNN kuchapisha video ya CCTV kutoka kwenye hoteli iliyokuwa ikifahamika kama Intercontinental huko Century City, Los Angeles.
Cassie anaonekana akiondoka haraka kwenye chumba walichokuwa na anafuatwa na Combs ambaye alikuwa amejifunga taulo. Combs anampiga kofi Cassie na kumpokonya mkoba wake na kisha kumburura sakafuni kwa kuvuta nywele yake.
Jana Jumapili, Combs alichapisha video ya msamaha kwenye akaunti yake ya Instagram ambapo alisema ni vigumu sana kuangazia matukio ya awali mabaya, lakini wakati mwingine inabidi.
“Nilikosea, nikajishusha sana lakini hicho sio kisingizio. Tabia yangu kwenye hiyo video haistahili kisingizio chochote.” alisema Diddy kwenye video hiyo.
Aliendelea kusema kwamba anawajibikia vitendo vyake kulingana na video hiyo akisema alichukizwa na navyo wakati huo na hata sasa na kwamba anajibidiisha kuwa bora kila siku.
Cassie alitengana na Diddy mwaka 2019 na mwezi Novemba mwaka jana aliweka kesi kortini dhidi ya Diddy kwa madai ya kumshambulia ambayo Diddy alikana ila sasa amekiri baada ya ushahidi kutplewa hadharani.
Wahusika kwenye kesi hiyo wanasemekana kuafikia makubaliano.
Baada ya kuona video ya Diddy ya kuomba msamaha, Meredith Firetog ambaye ni wakili wa Ventura, alitoa taarifa ambapo alisema kwamba Diddy anajifikiria mwenyewe katika msamaha huo na wala sio wengi aliowakosea.
Alielezea kwamba wakati Ventura na wengine walijitokeza na kulalamikia kushambuliwa na Diddy, alikana madai yote dhidi yake akisema kwamba walikuwa tu wanataka pesa kutoka kwake.