Viongozi na wazee katika eneo la Isiolo wametofautiana kuhusiana na operesheni ya usalama inayotarajiwa kutekelezwa katika eneo hilo.
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki ametangaza mipango ya kutekelezwa kwa operesheni hiyo.
Ingawa wazee kutoka jamii zilizoathirika zaidi na wizi wa ng’ombe wanataka operesheni hiyo kuanzishwa mara moja, viongozi kutoka maeneo yanayolengwa wanataka isitekelezwe ili kuwawezesha kuzungumza na wanachama wa jamii zao.
Aidha viongozi hao wanasema hatua hiyo itawezesha kurejeshwa kwa mifugo walioibwa na kufichwa katika jamii zao, na hilo lisipofanyika, basi operesheni hiyo inapaswa kuanza.
Akizungumza jana Alhamisi katika eneo la Mlango katika wadi ya Burat, kaunti ya Isiolo wakati wa hafla ya kukabidhiwa kwa zaidi ya ngamia 200 walioibwa katika kaunti ya Isiolo na kupatikana katika kaunti jirani ya Samburu, Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee wa Somali Idle Hassan alitaka operesheni hiyo kuanzishwa mara moja.
Alisema wale wanaotaka isianzishwe ili kutoa fursa ya kurejeshwa kwa mifugo walioibwa siyo wakweli bali wanataka tu kuchelewesha operesheni hiyo.
Viongozi wa kisiasa wakiongozwa na Gavana wa Isiolo Abdi Guyo walikuwa na maoni tofauti, wakiitaka serikali kuwapatia wazee na viongozi kutoka maeneo yanayolengwa muda zaidi wa kuwatambua wahalifu wanaojificha miongoni mwao na kurejesha mifugo wote walioibwa. Walisema hilo lisipofanyika, basi operesheni hiyo inaweza ikaanza kutekelezwa.
Viongozi hao wanasema ikiwa operesheni hiyo itatekelezwa, ni watu wasiokuwa na hatia hasa wanawake na watoto watakaothirika zaidi, huku wahalifu wakikimbia na kujificha.
Waziri Kindiki alisema pande zote ziliwasilisha hoja nzito akiongeza kuwa serikali itaridhia maombi yote na kuwaruhusu viongozi kuhakikisha mifugo walioibwa wanarejeshwa.
Hata hivyo, alionya kuwa operesheni hiyo haiwezi ikaepukika.