Oliech ataja anayestahili kuchukua mikoba ya Engin Firat

Francis Ngala
2 Min Read
Aliyekuwa nahodha wa timu ya Taifa Harambee Stars Dennis Oliech; Picha/kwahisani

Gwiji wa timu ya taifa Harambee Stars Dennis Oliech ametoa pendekezo lake la kocha mpya ambaye anaamini anaweza kuipeleka Kenya katika viwango vya kimataifa.

Kulingana na Oliech, kocha Francis Kimanzi ana uwezo wa kubadili mwelekeo wa timu ya taifa katika soka ya bara Afrika na kuipa timu ya nyumbani sura mpya.

Hisia za Oliech zinakuja saa chache kufuatia matokeo duni ya Harambee Stars katika michuano ya kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayoandaliwa nchini Morocco, mwaka 2025.

Nahodha huyo wa zamani wa Stars, ambaye alifunga mabao 34 katika mechi 76 ndani ya miaka 13 na kuwa mfungaji bora wa pili wa muda wote wa Kenya, alisema Engin Firat na benchi yake nzima ya ufundi wanafaa kutimuliwa.

“Benchi ya ufundi ivunjwe. Tumeona timu ikiripoti kambini kwa wakati na kufurahia maandalizi mazuri ya mchezo husika ili kupoteza tu. Tumempa Firat muda lakini matokeo hayajapatikana. Nadhani ni wakati wa kumuamini kocha wa humu nchini tena,” akasema Oliech.

Hata Hivyo, Oliech amempendekeza kocha Francis Kimanzi kuchukua mikoba ya Firat ili kuipeleka Kenya mbele.

“Kimanzi ndiye chaguo bora zaidi kurithi mikoba ya Firat, hakuna kocha mwingine aliyeifikisha timu katika kiwango alichofanya mwaka 2008. Amejidhihirisha kwa muda na anabobea katika kusaka vipaji, akifanya kazi na Salim, nina imani watafanya hivyo. Tafuta wachezaji wanaofaa na kujenga timu yenye uwezo wa kufika hatua ya mtoano ya AFCON 2027.”

Share This Article
Follow:
I am Versatile Multimedia Journalist with years of experience in Digital platforms, Live TV and Radio. In another world am a News Anchor and Reporter.