Ofisi za maeneo bunge kutumiwa kuendesha ushiriki wa umma

Martin Mwanje
2 Min Read

Karani wa Bunge la Taifa Samuel Njoroge amesema ofisi za maeneo bunge zitaanza kutumiwa kuandaa vikao vya ushiriki wa umma.

Njoroge amesema mipango inafanywa kuwezesha kutekelezwa kwa mpango huo.

“Katika juhudi za kuhakikisha ushiriki wa umma unakuwa bora na unakidhi kanuni zilizowekwa, Bunge la Taifa litatumia ofisi za maeneo bnge kuendesha vikao vya ushiriki wa umma,” alisema Njoroge wakati akiuhutubia mkutano wa viongozi wa Bunge la Taifa mjini Naivasha.

Mkutano huo wa siku tatu unaongozwa na Spika Moses Wetang’ula na kuhudhuriwa na miongoni mwa wengine kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah na mwenzake wa wachache Junet Mohamed.

Wetang’ula amesema vikao vya ushiriki wa umma vitaimarishwa punde mswada uliopendekezwa wa ushiriki wa umma utakapopitishwa bungeni.

“Mswada huo uliopendekezwa na ambao upo kwa Mwanasheria Mkuu utaziba mianya yote ya ushiriki wa umma ambayo imekuwa ikisababisha mkanganyiko katika mahakama zetu kila wakati kesi za kupinga vikao hivyo zinapowasilishwa mahakamani,” amesema Spika huyo wa Bunge la Taifa.

Ametoa wito kwa wabunge kuharakisha mchakato wa kuupitisha mswada huo.

Matamshi yake yanakuja wakati ambapo wengi wametilia shaka vikao vya ushiriki wa umma vinavyoandaliwa nchini kuhusiana na masuala mbalimbali ambayo ni muhimu kwa taifa.

Wengi wamedai vikao hivyo vinaendeshwa kwa njia ya kutilia shaka ili kuufumba umma macho.

Ushiriki wa umma ni mojawapo wa masuala ambayo Naibu Rais aliyebanduliwa madarakani na Bunge la Seneti Rigathi Gachagua ameyataja kuwa sababu ya kupinga kufurushwa kwake.

 

Share This Article