ODPP yamtaka Inspekta Jenerali kuharakisha uchunguzi wa mauaji ya Wakili Mbobu

Marion Bosire
2 Min Read
Renson Ingonga - Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma – ODPP imemwelekeza Inspekta Jenerali wa Polisi kuharakisha uchunguzi kuhusu mauaji ya wakili mashuhuri Matthew Kyalo Mbobu.

Mbobu alipigwa risasi hadi kufariki katika tukio la ufyatuaji risasi kutoka kwa gari lililokuwa likipita katika eneo la Karen, Nairobi.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari leo, ODPP imesema imeshtushwa na kuhuzunishwa na tukio hilo la kusikitisha, na kuungana na jamii ya wanasheria na wananchi wa Kenya kuomboleza kifo chake.

Bwana Mbobu, wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya, aliheshimika kwa mchango wake katika taaluma, utumishi wa umma, na mazoezi binafsi ya sheria.

Alitambulika sana kwa kazi yake ya kuendeleza na kuunda mafunzo na utekelezaji wa Sheria ya Ushahidi hapa nchini.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka, na kumwagiza Inspekta Jenerali kuhakikisha ushahidi wote muhimu unakusanywa kwa haraka na kwa mujibu wa sheria.

Taarifa ya kina kuhusu maendeleo ya uchunguzi inatarajiwa kuwasilishwa kwa ODPP ndani ya siku saba kwa ajili ya mapitio na hatua zaidi.

Wakati huo huo, DPP amekaribisha dhamira ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) katika kutafuta hak na kurudia wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama.

Wananchi wenye taarifa zozote muhimu wametakiwa kujitokeza na kusaidia katika uchunguzi unaoendelea.

ODPP imesisitiza tena kujitolea kwake kwa kuhifadhi utawala wa sheria na kuhakikisha usalama na heshima ya kila Mkenya, wakati taifa likikumbwa na huzuni kufuatia kifo cha mmoja wa wataalamu mashuhuri wa sheria.

Website |  + posts
Share This Article