ODM yaunga mkono mazungumzo ya kitaifa

Martin Mwanje
2 Min Read

Chama cha ODM kimeunga mkono kufanyika kwa mazungumzo yanayokusudia kuangazia masuala mbalimbali yanayolikumba taifa. 

Uamuzi huo umefikiwa leo Jumatano wakati wa mkutano wa wabunge wa chama hicho na pia kamati kuu ya kitaifa ya chama.

“Mkutano wa wabunge wa ODM (PG) na Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) leo umeazimia kuwa tunapaswa kuwa na mkutano wa kitaifa/mazngumzo ili kuangazia masuala ya muda mrefu yanayowakumba Wakenya,” ilisema taarifa fupi kutoka kwa ODM baada ya mkutano huo uliohudhuriwa na Raila Odinga ambaye ni kinara wa chama.

“Kwamba mazingira mazuri yanapaswa kubuniwa kwa manufaa ya mpango huu. Kila Mkenya anapaswa kuhusishwa.”

Msimamo wa ODM unakuja wakati wito wa kufanyika kwa mazungumzo hayo umesababisha kuzuka kwa nyufa miongoni mwa viongozi wa muungano wa Azimio.

Hatua ya Raila awali kuunga mkono mazungumzo hayo ilikumbana na pingamizi kutoka kwa viongozi kama vile Kalonzo Musyoka (Wiper). Martha Karua (Narc K) na Jeremiah Kioni (Jubilee), vyote ambavyo ni vyama wanachama wa Azimio.

Viongozi hao wanashikilia kuwa hawawezi wakashiriki mazungumzo na utawala wa Kenya Kwanza wanaodai umekuwa ukiwakandamiza Wakenya.

Rais William Ruto alikuwa wa kwanza kutoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa kuangazia masuala mbalimbali yanayolikumba taifa.

Kufuatia msimamo wa hivi punde wa ODM, inatazamiwa kwamba mawimbi makali ya migawanyiko huenda yakatishia kuelea kwa meli ya muungano wa Azimio.

Vijana wa Gen Z pia wamepuuzilia mbali miito ya kufanyika kwa mazungumzo hayo.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *