Serikali imezindua miradi kadha ya maji katika sehemu ya Masol eneo la Pokot ya kati katika juhudi za kukabili kero la wizi wa mifugo na mizozo ya mpakani.Miradi hiyo inayotekelezwa la halmashauri ya ustawi wa eneo la Bonde la Kerio KVDA,inalenga kuhakikisha kwamba kuna maji ya kutosha na lishe kwa mifugo ili kupunguza mizozo juu ya rasli mali.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa halmashauri hiyo ya KVDA,Dr. Sammy Naporos, kufunguliwa kwa vituo vya maji vya Kalas na Amuto pamoja na bwawa ndogo la Selenka kutachangia pakubwa kusitisha mizozo hiyo ya kila mara kati ya wafugaji wa jamii za Pokot na Turkana.
Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong alisema wodi ya Masol imekuwa ikishuhudia makabiliano hayo akiongeza kuwa uzinduzi wa vituo hivyo vya maji utaimarisha hali ya usalama katika sehemu hiyo.
Naibu wa chifu huko Amoler ,Daniel Ptios alisema juhudi hizo zitachangia pakubwa kudumisha amani miongoni mwa jamii zinazozozania maji na lishe.Aliongeza kwamba wanawake pamoja na watoto wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta maji,na uzinduzi wa miradi hiyo sasa utapunguza muda wa kutafuta maji kwa wakazi hao.
Kamishna wa kaunti ya Narok Kipkech Lotiatia amepiga marufuku usafirishaji wa punda katika eneo hilo.Akiongea wakati wa mkutano wa hadhara huko Ewaso Kidong kwenye mpaka kati ya kaunti hiyo na Kajiado,Lotiatia alitangaza kuwa kaunti hizo mbili zimekubaliana kuweka marufuku hiyo ya usafirishaji wa punda,akiongeza kuwa yeyote atakayepatikana akisafirisha punde bila kibali,atachukuliwa hatua za kisheria.
Lotiatia pamoja na mwenzake wa kaunti ya Kajiado, Taari Rwaria walielezea hisia zao kuhusu visa vinavyoongezeka vya kuchinjwa kwa punda.Lotiatia alisema punda wengi wamenaswa katika siku za hivi karibuni wakiwa wanasafirishwa kwenye barabara kati ya Bomet- Mulot- Narok na Suswa .
Aliongeza kuwa punda hao mara nyingi husafirishwa hadi sehemu ya Ewaso Kidong ambapo huchinjwa kwenye vichaka.Alitoa wito kwa wananachi kujihadhari na watu ambao wanataka kuwauzia nyama ya porini hasa wakati huu wa msimu wa krismasi ambapo mahitaji ya nyama huongezeka.
Wazazi kwenye kaunti ya Kakamega wametakiwa kuwekeza katika maisha ya baadaye ya watoto wao.
Mkurgenzi wa chama cha ushirika cha Invest and Grow(IG SACCO), Tobias Oriedo alisema kuwekeza katika watoto kunahakikisha kwamba mahitaji yao ya kielemu na kiafya yanashughulikiwa ipasavyo.
Akiongea wakati wa hafla iliyoandaliwa na wanachama wa chama hicho cha ushirika,Oriedo alikariri umuhimu wa kuweka akiba na kuwekeza katika familia.Alitoa wito kwa wazazi kuwashauri watoto wao na kuhakikisha wako salama hasa wakati huu wa likizo hii ndefu. Oriedo alitoa wito kwa watu wazima katika jamii wawe wakifanya mazoezi ya viungo katika juhudi za kuboresha afya yao.
Viongozi huko Garissa wameelezea hisia zao kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mihadarati katika eneo hilo.Akiongea wakati wa mkutano katika chuo kikuu cha Garissa, viongozi hao akiwemo mbunge wa Garissa mjini Dekow Mohamed,walisema maovu mengi ya kijamii hutokana na uhaba wa ajira.
Wakati wa mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na gavana wa Garissa Nathif Jama, mwakilishi wa kike Udgoon Siyad, alisema serikali imetilia umuhimu mafunzo ya vyuo vya anwai kama chombo muhimu cha kuimarisha maisha ya vijana kwa kuwapa ujuzi. Gavana Nathif Jama alisikitika kwamba vijana kwenye kaunti hiyo wanapuuza kujiunga na vyuo hivyo.
Mkurugenzi mkuu wa baraza la kitaifa kuhusu watu na mipango Dr. Mohamed Sheikh, alisema mkutano huo unafanyika wakati ufaao huku akiwahimiza vijana kujiunga na vyuo hivyo ili waweze kupata ujuzi wa kutosha kuajiriwa au kujiajiri.
UNAENDELEA KUTUSIKILIZA KUTOKA KBC RADIO TAIFA. KUMBUKA, UNAWEZA KUFUATILIA HABARI HIZI KUPITIA TOVUTI YETU….www.rediotaifa.kbc.co.ke
Kwa siku ya nne mfululuzo taifa la Georgia limekumbwa na maandamano na visa vya maafisa wa umma kujiuzulu,kutokana na uamuzi wa chama tawala nchini humo wa kuahirisha mashauriano ya taifa hilo kujiunga na muunagano wa Ulaya.
Huku maelfu ya raia wa nchi hiyo wakiandamana kwenye miji kadha,waziri mkuu Irakli Kobakhidze amesema wandamanaji hao wamepotishwa na upinzani huku akifutilia mbali wito kwa kuandaliwa kwa uchaguzi mpya nchini humo.Waziri huyo mkuu alithibitisha kwamba balozi wa nchi hiyo huko Amerika , David Zalkaliani, ni moja wa maafisa wakuu wa kibalozi wa Georgia waliojizulu kufikia sasa.Wandamanaji hao walijitokezwa kwa wingi hapo jana ambapo walikabiliana vikali na polisi nje ya bunge la nchi hiyo.
Serikali ya Georgia imekuwa ikikashifiwa na muungano wa Ulaya na Amerika kwa kuvuruga demokrasia nchini humo.
Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir ametangaza kuwa Mombasa iko tayari kuandaa makala ya 14 ya michezo ya mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.Michezo hiyo inatarajiwa kuanza Desemba 6 hadi Disemba 18 katika Uwanja wa Mbaraki.Waziri Chirchir alitangaza kuwa maandalizi ya michezo hiyo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miundombinu muhimu na msaada wa vifaa ili kuandaa hafla hiyo ya kifahari.
Mashindano hayo yatajumuisha wabunge wa mataifa ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Wenyeji Kenya, Rwanda, Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, Jamhuri ya Sudan Kusini, Uganda na Tanzania, pamoja na Tanzania. Michezo itakayochezwa ni pamoja na; gofu, soka, riadha, kuvuta kamba, mpira wa pete, mpira wa wavu, mpira wa vikapu na mchezo wa darts kwa watu wenye ulemavu.