Oburu Oginga azuru Chungwa House, akutana na maafisa wa ODM

Martin Mwanje
1 Min Read
Kaimu kiongozi wa ODM Oburu Oginga akiwa na maafisa wengine wa chama, Chungwa House

Kaimu kiongozi wa chama cha ODM Oburu Oginga ambaye pia ni Seneta wa Siaya leo Jumatatu ametembelea makao makuu ya chama hicho yaliyopo Chungwa House na kukutana na maafisa kadhaa wa chama. 

Waliokuwepo wakati wa mkutano huo mfupi ni pamoja na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, Mkurugenzi Mtendaji Oduor Ong’wen na Naibu Katibu Mratibu wa chama Ruth Odinga ambaye pia ni mwakilishi wa wanawake, kaunti ya Kisumu na dada yake aliyekuwa kinara wa chama hicho, Raila Odinga.

Maelezo ya kina ya kilichojadiliwa mkutanoni hayakubainika, ingawa Sifuna amekuwa mstari wa mbele kukosoa serikali ya Kenya Kwanza ambayo ODM ni mshirika.

Baadhi ya wanachama cha ODM hasa kutokea eneo la Nyanza, ngome ya kisiasa ya chama hicho, wanasema kamwe hawataondoka serikalini hata baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Oburu alitwikwa jukumu la kuwa kaimu kiongozi wa ODM kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.

Tangu kifo cha Raila Oktoba 15, kunao viongozi chamani, akiwemo mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, wanaomezea mate kuchukua uongozi wa chama hicho.

Wachanganuzi wa mambo wanasema kufuatia kifo cha Raila, huenda migawanyiko ikakithiri katika chama cha ODM.

Website |  + posts
Share This Article