Oburu Oginga ametangaza rasmi kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwa wakazi wa Bondo.
Tangazo hilo linafungua rasmi milango ya nyumba ya Raila kuwakaribisha waombolezaji, kuifariji familia hiyo.
Kulingana na tamaduni ya jamii wa Luo, zoezi hilo hujulikana ‘Tero ywak pacho’ maana yake ikiwa kupeleka kilio nyumbani.
Aidha tangazo hilo, lilifaa kupelekwa na Mama Ida, mkewe Raila Odinga, lakini kutokana na muda mfupi uliopo, ilimbidi Oburu kuingilia kati na kutekeleza shughuli hiyo.
Akizungumza wakati wa kutoa tangazo hilo, Oburu alisema Raila alianguka alipokuwa akitembea akiwa ameandamana na mtoto wake wa kike Winnie Odinga na dadake Ruth Odinga.
Seneta huyo wa Siaya ametoa wito kwa wananchi kudumisha utulivu, umoja na amani.
“tumehuzunika, tusipige makelele,” alisema Oburu.
Oburu ametangaza kwamba ibada ya mazishi ya Raila itaandaliwa katika uwanja was chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga.
Raila atazikwa karibu na makaburi ya wazazi wake huko Kang’o, Nyamira kwenye hafla itakayohudhuriwa na watu wachache.
Kang’o Ka Jaramogi huko Nyamira, Bondo, kaunti ya Siaya, ndiyo makao ya familia ya Odinga.
Makao hayo yana kaburi la marehemu Jaramogi Oginga Odinga na ploti za makaburi ya watu wa familia hiyo.