Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama na mkewe Michelle wamemuidhinisha Kamala Harris kugombea urais utakaoandaliwa nchini Marekani mwezi Novemba mwaka huu.
Harris anatarajiwa kuidhinishwa kuwa mgombea wa chama cha Democratic wakati wa mkutano wa chama hicho utakaoandaliwa Agosti 19-22 mjini Chicago.
“Mapema wiki hii, Michelle na mimi tulimpigia simu rafiki yetu Kamala Harris. Tulimuambia tunafikiri atakuwa Rais mzuri wa Marekani, na kwamba tunamuunga mkono kikamilifu,” alisema Obama kupitia mtandao wake wa X.
“Wakati huu muhimu kwa nchi yetu, tunaenda kufanya kila kitu kinachowezekana kuhakikisha anashinda mwezi Novemba. Tunatumai utaungana nasi.”
Harris ameendelea kupata uungwaji mkono wa wanachama wa chama cha Democratic tangu Rais Joe Biden kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Wakati akijiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho, Biden alimpendekeza Harris ambaye ni makamu wake kumrithi.
Ikiwa atateuliwa na chama cha Democratic, basi Harris atakabiliana na mgombea wa chama cha Republican ambaye pia ni Rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump kwenye uchaguzi wa mwezi Novemba.