Nyakang’o: Afisi ya Mdhibiti wa Bajeti haina fedha za kutosha

Tom Mathinji
1 Min Read
Mdhibiti wa bajeti Dkt. Margaret Nyakang'o

Mdhibiti wa Bajeti Dkt. Margaret Nyakang’o amesema afisi yake inakabiliwa na uhaba wa fedha, hali inayohujumu utekelezaji wa majukumu yake.

Alipofika mbele ya kamati ya kusimamia utekelezaji wa katiba, Dkt. Nyakang’o alisema afisi yake inapata takriban shilingi milioni 700 ambazo hazitoshi kuiwezesha kufuatilia na kutathmini shughuli mbalimbali katika kaunti zote 47 nchini.

Kulingana naye, afisi yake hutathmini madeni ambayo hayajalipwa, lakini akasema kuwa punde tu fedha zinapofika afsini mwake, huelekezwa kwa shughuli zingine.

Kutokana na uhaba wa pesa, Nyakang’o alisema kuwa afisi yake inaweza tu kufuatilia na kutathmini shughuli katika kaunti 21 kati ya 47.

Mchakato wa kufuatilia na kutathmini shughuli katika kaunti ulibainisha kukosa kuzingatiwa kwa kiwango kilichowekwa cha mishahara jumla ya wafanyakazi huku pesa zikitumika nje ya mkakati wa bajeti.

Akijibu swali kutoka kwa mbunge wa kaunti ya Kiambu Gathoni Wamuchomba, Nyakang’o alisema kuwa afisi yake haitathmini fedha kutoka kwa ushuru wa nyumba, huku akijitenga na usimamizi wa fedha hizo.

Nyakang’o analitaka bunge kurekebisha sheria ya mdhibiti wa bajeti na kuiruhusu afisi hiyo kuripoti kuhusu maendeleo ya kiuchumi na ada mbalimbali.

Share This Article