NTSA: Msako dhidi ya ukiukaji sheria za trafiki usiku utaendelea

Tom Mathinji
1 Min Read
NTSA imesema itaendeleza msako nyakati za usiku kukabiliana na ajali za barabarani.

Halmashauri ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA), imeapa kuendeleza msako dhidi ya ukiukaji sheria za trafiki nyakati za usiku kote nchini.

Kupitia mtandao wa X siku ya Ijumaa, halmashauri hiyo ilisema ilinakili visa 19 vya ukiukaji kanuni za trafiki katika barabara kuu ya  Nairobi – Nakuru Alhamisi usiku.

“Visa 19 vya ukiukaji wa sheria za trafiki ikiwa ni pamoja na uendeshaji magari  madereva wakiwa walevi, vilinakiliwa Alhamisi usiku katika barabara kuu ya Nairobi – Nakuru,” ilisema NTSA kwenye taarifa hiyo.

Aidha halmashauri hiyo iliwahimiza madereva kuwajibika kwa kuto-endesha magari wakiwa walevi, ili kuhakikisha usalama wao, wa abiria na watumizi wengine wa barabara.

“Kuwa dereva anayewajibika ni rahisi, ukiwa mlevi usiendeshe gari,” iliongeza NTSA.

NTSA ilisema kuwa msako nyakati za usiku utaendelea katika sehemu zote za nchi hadi pale ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva walevi zikatokomezwa.

Msako huo wa NTSA umejiri siku moja tu baada ya halmashauri hiyo kutoa takwimu kwamba watu wapatao 1,139 wamepoteza maisha yao kwenye ajali za barabarani kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu.

TAGGED:
Share This Article