Nitawashtaki Polisi, asema Bobi Wine

Tom Mathinji
1 Min Read
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine.

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine, leo Ijumaa amesema chama chake kitashtaki idara ya polisi, baada ya kujeruhiwa katika makabiliano na maafisa hao mapema wiki hii.

Wine, alisema alirushiwa kitoza machozi, wakati wa makabiliano hayo siku ya Jumanne.

Awali chama cha National Unity Platform (NUP), kilisema Wine mwenye umri wa miaka 42 ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, alipigwa risasi mguuni, huku polisi wakisema alijijeruhi mwenyewe.

“Tutawafungulia mashtaka hawa wahalifu ambao  ni maafisa wa polisi,” alisema mwanasiasa huyo katika mkutano na wanahabari nyumbani kwake Magere.

Wine alitaja tukio hilo kuwa jaribio la mauaji.

Wine aliruhusiwa kuondoka hospitali siku ya Jumatano baada ya kufanyiwa upasuaji.

Mwanasiasa huyo ambaye aliwania uchaguzi mkuu wa mwaka 2021, amefungwa na kuzuiliwa nyumbani kwake mara kadhaa, na pia mikutano yake ya siasa imevurugwa na maafisa wa usalama.

Share This Article