Nipo gizani kwa sababu ya ubabadume, adai Mwangaza

Martin Mwanje
2 Min Read
Gavana wa zamani Kawira Mwangaza akiwa mahakamani wakati wa kutolewa kwa uamuzi dhidi yake

Gavana wa zamani wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza sasa anadai kuwa wanasiasa wanaume kutoka kaunti hiyo walikula njama ya kisiasa ya kumtimua madarakani. 

Anasema wanasiasa hao, hawakuficha wajibu waliotekeleza katika kumtema, walipohuhudhuria uapisho wa mrithi wake juzi Jumatatu.

Mwangaza ameapa kutumia idara ya mahakama kupinga kwa udi na uvumba kung’olewa kwake madarakani akisema mchakato uliosababisha hatua hiyo ulijaa hadi pomoni dosari chungu nzima.

Gavana huyo wa zamani, ambaye aliwahi kuhudumu kama mwakilishi wa wanawake wa kaunti hiyo, pia hakuisaza serikali kuu katika masaibu yake.

“Serikali kuu, badala ya kudumisha utawala wa sheria, ilishawishi vilivyo matokeo kwa kuhakikisha kuwa sauti za wakazi wa Meru walionichagua zilitua kwa sikio la kufa,” alidai Mwangaza aliyezungumza kwa mara ya kwanza tangu kuapishwa kwa Naibu wake Isaac Mutuma kushika hatamu za kuiongoza kaunti hiyo.

Wiki jana, Mahakama Kuu iliridhia uamuzi wa mwaka jana wa Bunge la Seneti wa kumwondoa madarakani Mwangaza.

Uamuzi uliotolewa na Jaji Bahati Mwamuye ulipisha kuapishwa kwa Mutuma kuwa Gavana mpya wa kaunti ya Meru.

Mutuma ameapa kuwatumikia wakazi wa Meru kwa uadilifu wakati akihakikisha kuwa yeye ni nguzo itakayowaunganisha wanasiasa wa eneo hilo.

Wakati wa hafla ya uapisho wa Mutuma juzi Jumatatu, baadhi ya wanasiasa wa Meru wakiongozwa na mbunge wa Buuri Rindikiri Mugambi walielezea waziwazi wajibu waliotekeleza kuhakikisha mwanga wa Mwangaza madarakani unamezwa na giza kuu.

Wanasiasa wengi wa eneo hilo wamekuwa wakivutana na Gavana huyo wa zamani tangu alipoingia madarakani wakimtuhumu kwa kuwatenga katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kwa kutumia rasilimali za umma visivyo.

Mwangaza amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa kumbandua madarakani.

 

Website |  + posts
Share This Article