Nigeria imewakamata raia saba wa Poland kwa kupeperusha bendera za Urusi wakati wa maandamano dhidi ya serikali wiki hii katika jimbo la kaskazini la Kano, Peter Afunanya, msemaji wa idara ya usalama ya serikali, alisema Jumatano, Reuters imeripoti.
Mamia ya maelfu ya Wanigeria wamekuwa wakiandamana tangu Agosti 1 dhidi ya mageuzi yenye maumivu ya kiuchumi chini ya Rais Bola Tinubu ambayo yamesababisha mwisho wa kiasi cha ruzuku ya petroli na umeme, kushuka na mfumuko wa bei kufika viwango vya juu.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema maandamano hayo ambayo yalisababisha vifo katika takribani majimbo sita ya kaskazini yameshuhudia watu 22 wakiuawa wakati wa maandamano hayo, huku waandamanaji zaidi wakiuawa huko Kano.
Wiki hii, baadhi ya waandamanaji walipeperusha bendera za Urusi wakati wa maandamano katika majimbo ya kaskazini, kusisitiza wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa shughuli za Urusi magharibi mwa Afrika.
Idara za usalama ziliwazuia baadhi ya mafundi cherehani waliosema walikuwa wametengeneza mabango hayo.
Stanislaw Gulinski, balozi wa Poland nchini Nigeria, alithibitisha kukamatwa kwa watu hao katika mkutano kati ya waziri wa mambo ya nje wa Nigeria na wanadiplomasia katika mji mkuu, Abuja. “Walikamatwa siku mbili zilizopita huko Kano na mwisho nilisikia, walikuwa kwenye ndege kuelekea Abuja kutoka Kano,” alisema.