Nigeria walipoteza nafasi chungu tele na kulazimishwa kutoka sare ya bao 1 dhidi ya Equitorial Guinea katika mchuano wa kundi A uliochezwa Jumapili jioni katika uwanja wa Alassane Ouattara mjini Abidjan, Ivory Coast.
Iban Salvador aliwaweka Equitorial Guinea maarufu kama ‘national lightening’ kifua mbele kwa bao la dakika 36, akiunganisha pasi ya Jose Machin.
Hata hivyo, mshambulizi matata wa Super Eagles Victor Osimhen aliwakomboa Nigeria dakika mbili baadaye akiunganisha pasi ya Ademola Lookman.
Nigeria walibuni jumla ya nafasi 18 huku nane zikiwa mashambulizi ya moja kwa moja langoni lakini bado walinyimwa fursa ya kufunga bao lingine.
Ivory Coast wangali kuongoza kundi A kwa alama 3 wakifuatwa na Nigeria na Equitorial Guinea kwa alama 1 kila moja.