Viongozi wa kijeshi wa mataifa ya Niger, Mali na Burkina Faso, wametia saini mkataba mpya wa ushirikiano, katika hatua inayoashiria kujiondoa kwa nchi hizo kwenye miungano ya zamani.
Abdourahamane Tchiani kiongozi wa Niger, Ibrahim Traore wa Burkina Faso na Assimi Goita wa Mali walikutana Jumamosi katika jiji kuu la Niger, Niamey ambapo walitia saini mkataba wa kuunda chama cha kupiga jeki makubaliano yaliyoafikiwa mwaka jana ya ulinzi almaarufu “The Alliance of Sahel States – AES.
Kutiwa saini kwa mkataba huo kulihitimisha kongamano la kwanza la viongozi wa nchi hizo tatu ambazo zilikumbwa na mapinduzi ya kijeshi.
Maafikiano yanajiri miezi michache tu baada ya nchi hizo tatu kujiondoa kwenye muungano wa kiuchumi wa mataifa ya magharibi mwa Afrika – ECOWAS.
Akizungumza kwenye kongamano la Jumamosi, Tchiani aliutaja muungano wa ECOWAS ambao umekuwepo kwa miaka 50 kuwa tishio kubwa kwa nchi zao.
ECOWAS ilisimamisha uanachama wa nchi hizo tatu kufuatia mapinduzi ambayo yalitokea nchini Mali Agosti mwaka 2021, Septemba 2022 huko Burkina Faso na Julai 2023 nchini Niger.
Muungano huo uliwekea nchi hizo vikwazo pia na kutoa masharti ya kurejeshwa kwa uanachama wao.