Nicole Berry aachiliwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana

Mwigizaji huyo anakabiliwa na kesi ya kuhujumu uchumi kwa kukusanya pesa bila idhini.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji wa filamu nchini Tanzania, Joyce Mbaga maarufu kama Nicole Berry pamoja na mwenzake Rehema Mahanyu waliachiliwa kutoka korokoro za polisi baada ya kutimiza masharti ya dhamana.

Wawili hao wanakabiliwa na kesi ya kuhujumu uchumi kwa kukusanya pesa kutoka kwa umma bila idhini rasmi na dhamana yao ni shilingi milioni 100 pesa za Tanzania sawa na milioni 4.8 za Kenya.

Nicole na Rehema walifikishwa mahakamani mbele ya hakimu mkazi huko Kivukoni Kinondoni, Jumatatu Machi 10, 2025, ambapo walisomewa mashtaka yao ya kukusanya pesa bila kibali cha benki kuu ya Tanzania inavyohitajika kisheria.

Jana Jumatatu Machi 17, 2025 ndiyo siku waliachiliwa na hakimu mkazi mwandamizi, Ramadhani Rugemarila, anayesikiliza kesi hiyo, baada ya kutimiza masharti haya ya dhamana.

Nicole amedhamiwa kwa hati ya umiliki wa nyumba ya thamani ya shilingi milioni mia moja ya mdhamini wake ambaye jina lake halikuwekwa wazi.

Rehema naye alidhaminiwa na Ramadhan Juma, Joyce Isdon, na hatimiliki ya nyumba ya thamani ya shilingi milioni 57 za Tanzania sawa na shilingi milioni 2.7 za Kenya.

Marafiki hao wanadaiwa kuchangisha milioni 185.5 za Tanzania kinyume cha sheria na wakadaiwa kuendesha genge la uhalifu, makosa yaliyotekelezwa kati ya Julai 2024 na Machi 2025 ndani ya Mkoa wa Dar es salaam.

Kesi hiyo inapangiwa kusikiliwa Machi 24,2025 kulingana na maelezo ya hakimu ya tarehe 10 mwezi machi mwaka huu wa 2025.

Website |  + posts
Share This Article