Ashanti na mume wake ambaye pia ni mwanamuziki Nelly, walikwenda pamoja kuhudhuria tuzo za muziki za iHeartRadio katika ukumbi wa maonyesho wa Dolby huko Ovation Hollywood Jumatatu Machi 17, 2025.
Tuzo za muziki za iHeartRadio huwa zinatambua wasanii ambao miziki yao imechezwa mara nyingi kwenye vituo vya redio vya iHeartRadio nchini Marekani na kwenye app ya iHeartRadio.
Nelly hakujua kwamba Ashanti alikuwa mmoja wa watakaokabidhi washindi tuzo na kwamba yeye alichaguliwa kumkabidhi tuzo ya Landmark.
Akitoka walikokuwa wameketi, Ashanti alimdanganya Nelly kwamba anakwenda msalani na kisha akamshtukia akiwa jukwaani. Kabla ya kumpa tuzo hiyo, aliimba sehemu ndogo za nyimbo za Nelly kama Air Force Ones na Hot in Herre.
“Hakujua kwamba ninakuja haa juu, alifikiria nakwenda msalani.” alisema Ashanti huku akiendelea kumsifia Nelly kwa kuwa mwanamuziki bora wa mtindo wa Rap kutoka St. Louis, wakati wengi waliamini wanamuziki wengi wa mtindo huo walitoka pwani Mashariki na Magharibi.
Ashanti ambaye ana mtoto wa kiume na Nelly wa umri wa miezi saba pekee aliendelea kusema, “Mwaka huu ni wa 25 tangu alipozindua albamu yake ya kwanza ‘Country Grammar’ iliyoongoza chati kwa wiki sita mfululizo.”
Albamu hiyo ni mojawapo ya albamu za hip-hop ambayo iliuza nakala zipatazo milioni 10.
“Ninajivunia kuipa heshima Country Grammar na jamaa mwenye talanta ambaye aliitengeneza, mpenzi wangu, mume wangu Nelly, kwa tuzo hii la Landmark ya iHeartRadio.
Nelly ambaye alikuwa akitabasamu hakutoa hotuba ya kukubali tuzo hiyo.
Tuzo hii imejiri wakati Nelly anajiandaa kuabza ziara yake ya kikazi kama mwanamuziki ambayo ameipa jina la “Where the Part At” itakayoanza Machi 21 2025 huko New Zealand.
Ataandamana na wanamuziki kama Ja Rule, Eve, St. Lunatics, Fabolous, Jermaine Dupri na Chingy.