Mwanamuziki wa Marekani Jay Z amepata pigo baada ya jaji kutupiliwa mbali kesi ambayo alikuwa amewasilisha dhidi ya wakili Tony Buzbee.
Jay-Z ambaye jina lake halisi ni Shawn Carter alikuwa amewasilisha kesi dhidi ya Buzbee akimlaumu kwa kutaka kumnyang’anya pesa na kumharibia sifa.
Malalamishi ya Jay Z yalitokana na kesi ambayo iliwasilishwa mahakamani na Buzbee kwa niaba ya mwanamke fulani kutoka eneo la Alabama ambaye jina lake halikutajwa, aliyedai kudhulumiwa kingono akiwa na umri wa miaka 13.
Buzbee na wakili mwenza David Fortney walimtaja Jay-Z kuwa mshukiwa katika kesi hiyo ambayo baadaye ilimalizwa na mawakili wa Jay Z, waliowasilisha ushahidi mahakamani na kumlazimu mwanamke huyo kuondoa madai dhidi ya mteja wao.
Mwanamke huyo hata hivyo alidumisha malalamishi dhidi ya mwanamuziki P. Diddy katika kesi hiyo.
Jay Z aliwashtaki Buzbee na Fortney, akidai waliongozwa na ulafi kiasi kwamba hawakuzingatia ukweli na utu walipomtaja katika kesi hiyo.
Jaji Mark Epstein wa mahakama ya Los Angeles alitupilia mbali kesi hiyo katika uamuzi wake wa kurasa 65, ambapo alitambua ukiukaji wa maadili lakini akabainisha kwamba matendo ya mawakili hao hayakuafikia viwango vya kuorodheshwa kama utozaji wa kihalifu.
Mawakili wa Jay Z wamejibu uamuzi huo wakisema kwamba umewashtua na ni wa kukatisha tamaa, huku wakili Alex Spiro akifafanua kwamba wanapanga kukata rufaa.