Marudio ya nusu fainali za Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika yataandaliwa Ijumaa usiku, huku timu mbili zitakazocheza fainali ya msimu huu zikitarajiwa kubainika.
Washindi mara moja na mabingwa wa taji ya Afrika Football League,Mamelodi Sundowns watakuwa nyuma Pretoria, kuvaana na mabingwa mara nne Esperance kutoka Tunisia kuanzia saa tatu usiku.
Esperance wanaongoza bao moja kutokana na duru ya kwanza, huku ‘Masandawana’ wakihitaji ushindi wa magoli mawili kwa bila ili kutinga fainali.
Nusu fainali ya pili itasakatwa jijini Cairo kuanzia saa nne usiku kati ya mabingwa mara 10 Al Ahly, dhidi ya mabingwa mara tano TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Timu zote zilitoka sare katika mkumbo wa kwanza.
Washindi wa Jumla watafuzu kwa fainali kuwania kitita cha dola milioni 1.5 na fursa ya kushiriki Kombe la Dunia mwaka ujao nchini Saudi Arabia.