NGEC yalaani kushambuliwa kwa mjane Nyamira

Martin Mwanje
2 Min Read
Rehema Jaldesa - Mwenyekiti wa NGEC

Tume ya Taifa ya Jinsia na Usawa (NGEC) imelaani vikali kushambuliwa kwa mwanamke mmoja aliyekuwa akiomboleza kifo cha mumewe katika eneo la Nyabisimba, kaunti ya Nyamira. 

Mwenyekiti wa tume hiyo Rehema Jaldesa ametaja tukio kuwa ushahidi wa vurugu za kijinsia zinazokiuka haki za wanawake kwa kisingizio cha utamaduni.

“Dhuluma kama hizo ni ukiukaji wa kifungu nambari 27 cha Katiba ya Kenya, 2010, kinachohakikisha usawa na uhuru dhidi ya ubaguzi,” alisema Jaldesa kwenye taarifa.

NGEC sasa inatoa wito kwa jamii kuachana na tamaduni potovu zilizopitwa na wakati na kutumia njia za kisheria na mbadala kutatua migogoro kati yao.

Hadi kufikia sasa, washukiwa watatu wamekamatwa katika eneo hilo la Nyabisimba kwa madai ya kumdhulumu mwanamke huyo kwenye hafla hiyo ya mazishi.

Watatu hao ambao ni Robert Pokea Sarudi mwenye umri wa miaka 43, Bismark Ondiek Sarudi mwenye umri wa miaka 40 na Lameck Ogindo Osoro mwenye umri wa miaka 27, wanadaiwa kumlazimisha mwanamke huyo kushiriki tambiko la kitamaduni kinyume cha mapenzi yake, na hivyo kumdhulumu na kumsababishia mjane huyo majeraha ya kimwili.

Kisa hicho kilitokea Machi 21, 2025, wakati mwanamke huyo aliyekuwa ameolewa kwa muda wa miaka tisa na mume wake ambaye sasa ni marehemu, alijipata katika mzozo wa kifamilia.

Baada ya kutalikiana na mume wake, alifahamishwa kuhusu kifo cha baba huyo wa watoto wake na kuarifiwa awapeleke watoto wamzike baba yao, aliyefariki kupitia ajali ya barabarani.

Wakati wa mazishi, baadhi ya jamaa wa mwendazake walimlazimisha mwanamke huyo kushiriki tambiko la kitamaduni la kurusha mchanga kwenye kaburi, lakini alikaidi na hapo akaanza kushambuliwa akilaumiwa kwa kusababisha kifo cha mume wake.

Maafisa wa usalama walifahamishwa kuhusu kisa hicho na polisi wakaanza uchunguzi mara moja, na kusababisha kukamatwa kwa washukiwa hao watatu katika eneo la Mwongorisi.

Kwa sasa, washukiwa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kiambere, wakisubiri kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI kupitia ukurasa wa X, juhudi zinaendelea kuwasaka na kuwashtaki washukiwa zaidi wanaodaiwa kuhusika katika kisa hicho.

Website |  + posts
Share This Article