Netanyahu aashiria ujio wa mapatano mengine ya kuachiliwa kwa wafungwa

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameashiria kwamba huenda kukaafikiwa mapatano mengine ya kuachilia wafungwa wa pande zote mbili kwani mashauriano yanaendelea.

Aliyasema hayo jana Jumamosi kwenye mkutano na wanahabari uliopeperushwa moja kwa moja kwenye runinga akitaja vita vinavyoendelea kuwa vita vya uwepo.

Kulingana naye vita hivyo ni lazima vipiganwe hadi ushindi upatikane hata ingawa kuna changamoto za shinikizo na gharama. Alisema Gaza itapokonywa jeshi na itakuwa chini ya ulinzi wa Israel.

Matamshi yake yalijiri siku moja baada ya wanajeshi wa Israel kuua kimakosa mateka watatu kati ya wote ambao ni zaidi ya 100.

Netanyahu alisema kwamba mashambulizi ya Israel huko Gaza yalisaidia kuafikiwa kwa mkataba wa muda wa kuachiliwa kwa baadhi ya mateka mwezi Novemba huku akiahidi kuendeleza mashambulizi hayo dhidi ya Hamas.

Haya yanajiri baada ya mkuu wa shirika la ujasusi la Israel linalofahamika kama Mossad, kukutana na waziri mkuu wa Qatar, nchi inayoongoza mashauriano kati ya Israel na Hamas.

Juhudi za Qatar zilisababisha kuafikiwa na kutekelezwa kwa mapatano ya kusitisha vita kwa siku saba na kuachiliwa kwa baadhi ya mateka.

Qatar pia ilithibitisha kwamba majadiliano yanaendelea kuhusu kuafikia kwa mapatano mengine.

Netanyahu alikwepa swali kuhusu mkutano unaosemekana kufanyika Uingereza lakini alithibitisha kwamba alitoa maagizo kwa kundi linalohusika kwenye majadiliano.

Kiongozi huyo alisema wana ukosoaji mkubwa dhidi ya Qatar lakini la muhimu kwa sasa ni kuafikia kuachiliwa kwa mateka wa nchi yake.

Baadaye kundi la Hamas lilitoa taarifa iliyosema kwamba haliko tayari kuhusika kwenye mazungumzo ya kubadilishana wafungwa wa vita iwapo mashambulizi dhidi ya watu wao hayatasitishwa kabisa.

Website |  + posts
Share This Article