Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Maridhiano, NCIC imekita kambi katika kaunti ya Garissa ambako makabiliano kati ya makabila ya eneo hilo yamechacha.
Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, mashambulizi ya kulipiza kisasi yamesababisha vifo vya watu 13.
Wanafunzi sita ni miongoni mwa waliouawa kwa kupigwa risasi wakati wakiwa wameabiri gari aina ya probox katika eneo la Kunaso wakielekea katika mji wa mpakani wa Holugho.
Katika juhudi za kutuliza hali, NCIC imechukua hatua ya kufanya mikutano na washikadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na maafisa wa serikali ya kaunti, maafisa wa usalama, wazee wa kudumisha amani na viongozi wa kidini kwa lengo la kutafuta suluhu ya kudumu kwa makabiliano ambayo yameshuhudiwa kati ya makabila ya eneo hilo.
Tume hiyo imewaonya raia dhidi ya kueneza semi za chuki kwenye mitandao ya kijamii, ikiongeza kuwa watu wanaopachika jumbe za chuki kwenye mitandao hiyo watakamatwa mara moja na kufunguliwa mashtaka mahakamani.
NCIC inasema itahakikisha hili linafanyika kwa kushirikiana na Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI na raia ambao wameshauriwa kuwasilisha jumbe za chuki zilizopachikwa kwenye mitandao ya kijamii kwa tume hiyo ili hatua ichukuliwe.
Kamishna wa tume hiyo Abdiaziz Farah amesema punde watakapopata ushahidi ama kwa njia video au picha zilizopigwa za jumbe hizo, watachukua hatua haraka na kuwawajibisha wanaozieneza.
“Tunafahamu kwamba kuna semi nyingi za chhuki zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii. Hili halifanywi tu na watu wa Garissa bali pia watu waliopo nje ya nchi. Pia tumeambiwa kwamba baadhi ya watu wanatuma pesa kutoka nje ya nchi kufadhili tatizo hili,” alisema Farah wakati akiwahutubia wanahabari mjini Garissa baada ya kukutana na viongozi wa kidini.
Alisema uchunguzi unaendelea kubaini ukweli wa madai kwamba baadhi ya watu wanafadhili makabiliano hayo kutoka ng’ambo.
Kwa upande wake, kamishna Danvas Makori alisema watafanya kazi na vyombo vya usalama, tume ya kitaifa ya ardhi na serikali ya kaunti hiyo kutatua suala hilo, na kutoa wito wa kudumishwa kwa amani miiongoni mwa raia.
Viongozi wa kidini waliozungumza wakati wa mkutano na makamishna hao walisema chanzo kikuu cha uhasama katika mji wa Garissa ni ardhi na kutoa wito kwa serikali ya kaunti kuchukua hatua ya haraka na kuupanga mji huo ipasavyo.
Tayari, serikali ya kaunti imepiiga marufuku shughuli za uchimbaji madini na ugavi au uuzaji wa mashamba mjini humo.