NCIC yashtumu mapigano katika mpaka wa Kisumu na Kericho

Tom Mathinji
1 Min Read
Ghasia zazuka katika mpaka wa Kaunti za Kisumu na Kericho. Picha/Hisani

Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Maridhiano, NCIC imeshtumu vikali mapigano yaliyoshuhudiwa katika mpaka wa kaunti za Kisumu na Kericho. 

Watu wanane wameuawa na 18 kujeruhiwa kwenye mapigano hayo.

Katika taarifa, tume hiyo ilitoa wito kwa wanasiasa wa kaunti hizo mbili kuwatuliza wafuasi wao ili kusitisha uhasama baina yao.

“Tunatoa wito kwa wakazi wa kaunti hizo mbili kutumia mbinu zilizopo za kusuluhisha migogoro,” ilisema NCIC.

Aidha tume hiyo iliitaka Wizara ya Usalama wa Kitaifa kuimarisha usalama katika eneo hilo ili kuzuia kupotea kwa maisha zaidi na uharibifu wa mali.

Ili kuhakikisha wakazi wa kaunti hizo mbili wanaishi kwa amani, tume hiyo imesema imeanzisha mpango wa kushughulikia ugawanaji rasilimali zilizopo, uhasama wa kijamii, na miegemeo ya kisiasa.

Kamishna wa kaunti ya Kisumu Hussein Alassow Hussein alisema uchunguzi umeanzishwa kubaini kiini cha ghasia hizo huku akisema watakaopatikana na hatia watachukuliwa hatua kali.

Afisa huyo wa utawala alisema hakuna mshukiwa aliyekamatwa kufikia sasa japo maafisa wa usalama wamepelekwa katika sehemu hiyo kushika doria.

 

Website |  + posts
Share This Article