NCIC yaonya dhidi ya semi za chuki, wahusika kuwajibishwa

Tume hiyo imesema yeyote atakayepatikana akijihusisha katika uovu huo atachukuliwa hatua kali za kisheria bila kujali hadhi yake katika jamii.

Martin Mwanje
2 Min Read
Mwenyekiti wa NCIC Kepha Omae akiwa na makamishna wengine wakati wakiwahutubia wanahabari

Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC), imeonya vikali dhidi ya matumizi ya semi za chuki hususan kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. 

Mwenyekiti mpya wa tume hiyo Dkt. Kepha Omae ametaja hulka hiyo kuwa hatari kwa mshikamano wa kitaifa.

“Tunalaani vikali, aina zote za semi za chuki, kikabila, uchochezi wa kisiasa, na semi za kuchochea vurugu bila kujali miegemeo ya kisiasa, hadhi katika jamii, au hadhi ya kisiasa ya wahusika,” alisema Dkt. Omae katika mkutano wake wa kwanza na wanahabari tangu alipochukua hatamu za kuiongoza tume hiyo.

“Hakuna sababu za kisiasa, haijalishi zinashabikiwa kiasi gani, zinahalalisha kudunisha raia mwenzako. Hakuna dhamira za kisiasa zinapaswa kutumiwa kuchochea uhasama wa kikabila. Hakuna malalamishi, yawe halali au la, yanapaswa kutumiwa kuchochea vurugu dhidi ya mtu yeyote au jamii.”

NCIC imelaani matumizi ya semi za chuki wakati ambapo Katibu Mkuu wa chama cha UDA Hassan Omar anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu kwa madai ya kutoa semi za kikabila zinazoilenga jamii fulani nchini.

Tume hiyo inasema tume hiyo inamchunguza Omar kwa tuhuma za kutoa semi za uchochezi wa kikabila.

Seneta huyo wa zamani wa Mombasa amejitetea akisema semi zake zilifasiriwa visivyo ila ameomba msamaha kwa wale ambao huenda ziliwakwaza.

NCIC pia imeonya dhidi matumizi ya mitandao ya kijamii kueneza semi za chuki na kuwagawanya Wakenya ikisema wahusika watakiona cha mtema kuni.

 

Share This Article