Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Maridhiano, NCIC imeelezea mashaka juu ya joto la kisiasa linalozidi kupanda nchini.
Tume hiyo sasa inatoa wito kwa Wakenya kudumisha umoja wa taifa na kutotekwa nyara na mawimbi ya kisiasa yanayorindima nchini kwa wakati huu.
“NCIC ina wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali ya sasa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini Kenya,” amesema mwenyekiti wa tume hiyo Dkt. Samuel Kobia katika taarifa.
“Kile ambacho kimefanyika katika siku za hivi karibuni kimeathiri kwa njia hasi mshikamano na umoja wa jamii.”
NCIC sasa inatoa wito kwa Baraza la Madhehebu mbalimbali ya Kidini (IRCK) na Baraza la Taifa la Wazee kutenga Oktoba 10 kuwa siku ya kuliombea taifa hili na kuomba toba kutoka kwa Maulana kuhusiana na hali ilivyo nchini kwa sasa.
Kauli za NCIC zinakuja wakati hoja maalum ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua imesababisha migawanyiko miongoni mwa Wakenya huku baadhi wakiiunga mkono na wengine kuipinga.
Baadhi ya viongozi wa kidini wametoa wito kwa Rais William Ruto kuridhiana na Gachagua kwa ajili ya kukuza mshikamano wa taifa.
Bunge kwa sasa linajadili hoja maalum iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse kwa lengo la kumbandua Gachagua kutoka kwenye wadhifa huo.