Naibu Gavana wa kaunti ya Meru Isaac Mutuma alihojiwa kwa zaidi ya saa nne jana Jumatano na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI wa kaunti hiyo.
Mutuma alihojiwa kuhusiana na rabsha zilizoshuhudiwa wakati wa mkutano ulioandaliwa na Gavana Kawira Mwangaza katika eneo la Makiri, eneo bunge la Igembe Kusini Jumapili juma lililopita.
Mutuma ambaye amekuwa akizozana kwa muda mrefu na Gavana Mwangaza anatokea eneo hilo.
Akizungumza jana Jumatano usiku baada ya kuhojiwa na maafisa wa DCI kuhusiana na rabsha hizo, Mutuma alimkashifu Gavana Mwangaza kwa kukosa miradi inayonufaisha mwananchi.
Alidai Gavana huyo amepalilia mbegu za uhasama na kila kiongozi aliyechaguliwa katika kaunti ya Meru.
Uhasama wa kisiasa unazidi kurindima katika kaunti ya Meru huku kambi mbili kinzani zikiendelea kurushiana cheche za maneneo.
Mkutano wa Gavana Mwangaza eneo la Igembe Kusini ulisambaratika Jumapili juma lililopita baada ya vijana wenye hasira kuvuruga mkutano huo katika kile kinachoonekana kuwa ubabe wa kisiasa kati ya Gavana Mwangaza na Naibu wake.
Mkutano huo uliandaliwa chini ya mpango wa Gavana kwa jina “Okolea” ambapo alikuwa amepanga kugawa magodoro na kuipatia familia moja ng’ombe wa maziwa.
Baadhi ya wakazi walioghadhibika waliandamana hadi eneo la mkutano na kuripotiwa kuchoma magodoro hayo na kisha kumchinja ng’ombe huyo na kugawana nyama.
Maafisa wa polisi walilazimika kutumia vitoza machozi kutuliza hali.