NACADA, polisi wanasa mihadarati Molo

Tom Mathinji
1 Min Read

Operesheni ya pamoja iliyotekelezwa Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Mihadarati (NACADA) na Maafisa wa Huduma ya Taifa ya Polisi, imesababisha kunaswa kwa bangi ya thamani ya shilingi milioni moja katika kaunti ya Molo.

Mihadarati hiyo ilinaswa Jumatatu usiku, baada ya maafisa hao kunasa gari lililokuwa likiisafirisha katika eneo la Munju.

Kulingana na NACADA, operesheni hiyo ilimlenga mlanguzi huyo ambaye anaaminika alikuwa akisafirisha kiwango kikubwa cha mihadarati.

Maafisa hao walipojaribu kulisimamisha gari hilo, dereva alitoroka na kusababisha maafisa hao kulifuata.

Aidha, dereva aliangusha magunia matatu nje huku akitoroka bila kupatikana.

Afisa Mkuu Mtendaji wa NACADA  Dkt. Anthony Omerikwa, aliwashukuru wananchi kwa kuwapasha maafisa habari, akidokeza kuwa mamlaka hiyo imejitolea  kutokomeza matumizi ya mihadarati humu nchini.

Share This Article